Mamlaka Wajibu wa Chama

(i) Mamlaka

Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge (Mwenge Housing Cooperative Society Limited) kiliandikishwa mwaka 1971 na Wizara ya Kilimo na Vyama vya Ushirika ikishirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini. Chama kiliandikishwa katika Daftari ya Serikali tarehe 29.06.1971 kwa mujibu wa sheria za Vyama vya Ushirika ya mwaka 1968 na kupewa Hati Na. 2028.

Mnamo mwaka 1975, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa. Baadaye pia zilitungwa sheria za Vyama Vya Ushirika Na. 14 ya 1982, Na. 15 ya 1991, Na. 20 ya 2003, na Sheria Na. 6 ya mwaka 2013.

Sababu kuu ya marekebisho ya masharti ya mwaka 2016 ni kufanya masharti ya Chama yaendane na Sheria Na. 6 ya mwaka 2013 na Kanuni za Vyama vya Ushirika za mwaka 2015, pamoja na mazingira mapya ya uendeshaji wa Ushirika nchini na duniani.

(ii) Wajibu wa Chama

Wajibu wa Chama ni kurahisisha upatikanaji wa nyumba bora na nafuu kwa ajili ya wanachama, kuwatia moyo wanachama ili wajijengee wenyewe nyumba bora za kuishi, kuendeleza na kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo, na kujenga moyo wa ushirikiano na kusaidiana. Ili kutimiza sababu hizi, Chama kitafanya mambo yafuatayo:

  1. Kupata, kununua, kumiliki, kutunza, na kuendeleza ardhi kwa madhumuni ya wanachama kujijengea nyumba kwa ajili yao binafsi au kwa matumizi ya jumuiya.
  2. Kumwezesha kila mwanachama kupata Hati ya muda mrefu (Certificate of Occupancy) ya kumiliki kiwanja kilipojengwa nyumba yake.
  3. Kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za Chama.
  4. Kununua/kupangisha nyumba kwa ajili ya matumizi ya Chama na wanachama.
  5. Kutafuta ardhi, kuipima, na kupata viwanja ili kujenga nyumba kwa ajili ya wanachama au biashara.
  6. Kujenga nyumba kwa ajili ya matumizi binafsi au familia na majengo mengineyo kwa ajili ya viwanda, biashara, au matumizi ya jamii. Nyumba za aina hii zinaweza kuuzwa au kupangishwa kwa kufuata taratibu za kisheria.
  7. Kutoa vifaa kwa ajili ya ujenzi.
  8. Kupata, kununua, na kumiliki mali muhimu kwa kuendeleza mafanikio na madhumuni ya Chama.
  9. Kusimamia na kutunza mali za Chama (k.v. viwanja vya makazi, viwanja vya biashara, na nyumba zilizopo na zitakazojengwa) ili ziwe katika hali nzuri, na kutunga kanuni na masharti yahusuyo mali hizo.
  10. Kutunga sera na kanuni mbalimbali kutokana na mahitaji ya Chama.
  11. Bodi itakuwa na mamlaka ya kuunda Kamati mbalimbali kuendana na mahitaji ya Chama.
  12. Kutunza na kuhifadhi mazingira ya eneo lote linalomilikiwa na Chama cha Ushirika na maeneo ya wanachama.
  13. Kufanya lolote lile linalohusiana na uchumi na ustawi wa wanachama kulingana na Sheria Na. 6 ya mwaka 2013 na Kanuni za mwaka 2015 za Vyama vya Ushirika.
  14. Kuwawezesha wanachama kupata mikopo kwa ajili ya kujijengea nyumba za makazi.
  15. Kuwawezesha wanachama kujenga nyumba bora, kuinua kipato, na kukuza hali ya maisha.
  16. Kuwasisitiza wanachama kujiwekea akiba kwa ajili ya maendeleo ya baadaye.